Tuangalie biashara 21 za mtaji mdogo usiozidi tshs. 100,000 unazoweza kufanya na zenye faida kubwa. Mtaji mkubwa unaohitajika unapoanzisha biashara ni muda na wala sio pesa kama utakavyojifunza hapa.
Mimi binafsi siamini kama kuna biashara ndogo, ila najua kuna biashara unaweza kuanza na mtaji mdogo na zikakuletea faida kubwa.
Hiyo ambayo inaitwa “biashara ndogo” ukiifanya kwa ubora wa hali ya juu na bidii ipo siku itakutoa.
Nilipokuwa narudi mazoezini asubuhi ya leo, nilijiuliza je ni biashara gani unaweza kuanza na mtaji mdogo (isiyozidi laki moja)?
Nilijua zipo ila sikufikiria kama zinaweza kuleta faida nzuri tu utakapo zifanya kwa ubora.
Hivyo, nikaanza kuziandika kwenye simu na baada ya dakika chache nikajikuta nina orodha ya bishara zaidi ya ishirini unazoweza kuanza na mtaji mdogo na zenye faida kubwa ambazo nitaziandika hapa chini.
Kabla hatujaenda kwenye hiyo orodha ya hizo bishara za mtaji mdogo, ningependa kuweka sawa maana yangu ninaposema “zenye faida kubwa”.
Faida kubwa haimaanishi mamilioni ya fedha, bali ni kwamba faida utakayoipata kulingana na mtaji wako ni nzuri na usipokata tamaa zitakufikisha mbali.
Zingatia: unapotaka kuanzisha biashara yoyote ile, ni vyema kufuatilia utaratibu na sheria za mahali ulipo. Tafadhali ilinde biashara yako kwa kufuata kanuni zote zilizowekwa na serikali.
Baada ya kulisawazisha hilo, twende kwenye hiyo orodha ya biashara za mtaji mdogo kama zifuatazo;
1. Kupika kwa oda
Kama wewe ni mpishi mzuri au una mtu anayejua kupika, basi jitangaze kama unapokea oda za mapishi fulani.
Tuchukulie unaweza kupika makande au wali nyama vizuri.
Unachoweza kufanya ni kwenda maofisi ya karibu yako na kuwaambia kwamba wakutafute wanapohitaji hicho chakula wakati wa mchana na wewe utawaletea.
Usisahau kuacha mawasiliano yako ili waweze kukutafuta.
Wengi wao watapenda hiyo huduma kwasababu hawatohitaji kutoka tena kufata chakula.
2. Urembo (makeup, kusuka & kucha)
Urembo ni gharama. Wanadada wanataka kupendeza wanapokwenda safari zao kama ni kazini ama shughulini.
Uzuri ni kwamba hii ni biashara ya kila siku unayoweza kufanya.
Baada ya kufanya utafiti wangu, nimebaini kwamba kufanya makeup, kutengeneza kucha na ususi wa nywele zinalipa vizuri tu.
Kuna watu wengi tu wanaendesha maisha yao kupitia biashara hizo. Kwanini wewe ushindwe? Na kama sio mtaalamu, hakuna tatizo.
Chukua muda wako na kujifunza, ndani ya muda utaweza.
3. Kuuza juisi na icecream
Kujifunza kutengeneza juisi au icecream haitakuchukuwa muda mrefu. Ili kufanikiwa katika biashara hii, cha muhimu ni kujitofautisha.
Muhimu zaidi unapofanya biashara ya kutengeneza juisi au icecream, ni kuweka mazingira yako safi na salama kwa wateja wako.
Uzuri wa biashara hii ni kuwa mtaji wake ni mdogo sana.
Elfu kumi tu inatosha kuanzia na wapo waliofanya hivyo na wamekuza biashara zao kama vile mak juice au zanana juice box.
4. Kilimo cha mbogamboga
Kilimo ni sehemu kubwa ya maisha ya watanzania na wale wa nchi nyingi za afrika.
Kila siku zikienda, kilimo huzidi kuwa ni biashara ya matajiri kwasababu shamba lina gharama kubwa.
Licha ya hivyo, bado kuna fursa ya kutengeneza kipato kupitia kilimo cha mbogamboga hata kama una mtaji mdogo.
Anza na sehemu ndogo tu unayoweza kupata hata kama ni nyumbani.
5. Ufugaji wa ndege (kuku, bata, n.K)
Hii ni biashara ambayo ina faida kubwa lakini pia ina changamoto zake kama vile kuku wako kufa.
Vifo vya mifugo huwaumiza sana wafugaji na mara nyingi husababishwa na mifugo hiyo kula uchafu.
Hivyo, unapoingia kwenye ufugaji jitahidi uwe na mazingira safi na salama kwa mifugo yako.
Usafi wa mara kwa mara hasa hasa kwenye malisho yao utahitajika.
Kwa vile mtaji ni mdogo, unaweza kuanza na kuku wa kienyeji, bata au hata njiwa. Japo kuwa wanachukuwa muda ila kuwa mvumilivu, faida utaiona.
6. Kupiga picha
Tangu kuja kwa mitandao ya jamii kama vile instagram, watumiaji wa mitandao hiyo hutaka picha nzuri.
Hapo ndipo unapojitokeza wewe na kuwapa huduma yako ya kupiga picha.
Upigaji wa picha ni fani kama fani yengine, ili ujitofautishe pendelea kujifunza kwa wanaojua au tumia youtube kujifunza.
Vifaa vya upigaji picha vina gharama ila sio lazima viwe vyako, muhimu ni kuwa na ujuzi. Vifaa unaweza kumuazima rafiki yako au kukodi.
7. Kutengeneza tovuti (websites)
Tuko katika ulimwengu wa habari na teknolojia, hivyo kampuni ama biashara ambayo hawako mtandaoni wanakosa wateja.
Ichangamkie fursa hiyo kwa kujifunza kutengeneza websites kupitia youtube.
Kisha, tafuta biashara/ makampuni ambayo hawana tovuti na uwaelezee umuhimu wa kuwa na tovuti.
Mwisho, waambie kuwa wewe unatoa huduma hiyo.
Kwa kuanza, wateja wako wa mwanzo unaweza kuwafanyia kwa bei ya punguzo halafu mbeleni ukapandisha. Njia hii itakusaidia kupata mabalozi watakao kupatia wateja wengine.
8. Kupanga sherehe/matukio (event planning)
Kuanzia maharusi, kitchen party, sandoff na sherehe nyenginezo nisizozifahamu. Zote hizi ni fursa ambapo unaenda kusaidia watu kuandaa sherehe zao mwanzo mpaka mwisho.
Wewe ndio unaumiza kichwa kutafuta watu na huduma mbalimbali kama vile wapambaji, ma dj, au kuwatafutia gari ya kukodi, kuwapikishia chakula na megine mengi.
Unachohitaji kuweza kufanya biashara hii ni uwe unawajua watu husika wanaotakiwa kwenye sherehe hizo.
Mfano, ujue wapambaji wa ukumbi, wapishi wa maharusi, ma dj ili uweze kuwapa kazi hizo. Utalipwa kwa kufanya kazi hiyo.
9. Kutembeza watalii
Hii nayo ni biashara nyengine ambayo haihitaji pesa kabisa.
Unachohitaji ni kufahamu historia ya nchi yako hasa hasa ile ya maeneo ambayo watalii wanapenda kwenda.
Mfano, zanzibar mtembeza watalii anaweza kulipwa kuanzia elfu ishirini kwa safari moja. Kwa siku ukipata safari tano tu unaondoka na zaidi ya laki moja.
10. Ushonaji nguo
Kama wewe ni mpenzi wa mitindo, unaweza tengeneza kipato kizuri kwa kuwashonea watu nguo.
Itakuchukuwa muda kujifunza kushona ila ni kazi moja nzuri. Unapata kuwa mbunifu katika kutengeneza mishono mbali mbali na mwisho wake kulipwa.
Kama huna cherehani nyumbani, unaweza kwenda kukodi na kufanyia kazi zako hadi utakapo nunua yako.
11. Kufundisha
Unaweza kufundisha chochote kila unachokijua ikiwa kuna watu wanataka kujifunza.
Jitathmini kwa kujiuliza, je ni kitu gani nakijua ambacho watu wanataka kujifunza? Hiyo ni rasilimali tosha.
Watafute hao watu na uwape huduma zako. Taaluma sio lazima iwe kufundisha hesabati na kemia tu, kama unajua kupika vizuri, kushona au chochote kile basi wafundishe watu.
12. Kutengeneza simu/kompyuta
Watumiaji wa vifaa kama vile simu na kompyuta huzidi kila siku.
Vifaa hivi vinapopata tatizo kama vile kuingia loki sio kila mtu anaweza kutengeneza mwenyewe.
Hiyo hukupa wewe fursa ya kuwatatulia matatizo yao kwa kiasi cha pesa kadhaa. Unaweza kujifunza jinsi ya kutengeneza matatizo sugu ya simu kwenye mtandao.
13. Unyozi wa nywele
Hii pia ni biashara isiyokuwa na msimu kwavile nywele huota kila siku.
Jifunze kunyoa watu nywele halafu anza na wale wakaribu yako kama vile marafiki na ndugu.
Utakapofanya kazi nzuri hao watakuwa wateja wako wakujirudia na pia kukutangazia huduma zako kwa watu wengine.
Unachohitaji ni kununua mashine ya kunyolea ambayo unaweza kupata kwa chini ya elfu hamsini.
14. Kununua na kuuza bidhaa
Sifa ya kubwa ya mjasiriamali ni kuona thamani ya vitu kabla wengine hawajaviona.
Hivyo, tafuta bidhaa ambazo zinauzwa kwa bei ya chini, zinunue na utafute soko ambalo hizo bidhaa zinauzwa kwa bei ya juu uende ukaziuze huko.
Mfano, unaweza kutoa bidhaa dar es salaam ukaja kuuza zanzibar na kinyume chake pia inawezekana.
15. Kuuza vocha za simu
Vocha! Tunanunua karibia kila siku.
Faida yake sio kubwa kihivyo ila ukizingatia kazi ni ndogo ya kufanya kwasababu vocha zinajiuza wenyewe.
Vocha sio kitu cha kutumia nguvu kuuza muhimu watu wajue tu kama unauza vocha.
Unaweza kuona vocha zinauzwa kila sehemu kwamba utakosa wateja … lakini sio kweli, kuna sehemu nyingi tu ambazo hakuna muuza vocha karibu.
Anza kuwauzia watu unaoishi nao, majirani au hata wanafunzi wa chuo.
16. Ufugaji wa samaki
Ufugaji wa samaki uko wa aina mbili, kuna samaki wa kula na wale wa mapambo. Hapa nitaongelea samaki wa mapambo kwa vile wana gharama ndogo na pia faida kubwa.
Unaweza anza na samaki wawili au wanne na kuwatunza. Wakizaliana na kuwa wengi, uza baadhi yao
.
17. Kukuza miti ya maua
Maua hupendezesha nyumba na wengi huamua kupanda nyumbani kwao.
Fuatilia jinsi gani maua tofauti yanavyopandwa na kisha yapande.
Kwa wastani, mti mmoja wa maua huuzwa kuanzia elfu mbili. Mtaji mkubwa hapa ni muda wa kupanda na kuishughulikia hiyo miti.
18. Kufanya usafi majumbani na maofisini
Watu wengi wamebanwa na kazi, na muda wasiokuwa kazini wana mambo mengi ya kufanya.
Unaweza kuwafanyia usafi na wakakulipa. Ni vizuri ukanunua vifaa vyako ambavyo sio ghali ila sehemu nyingi watakuruhusu kutumia vifaa vyao vya usafi.
Biashara ikiwa kubwa, unaweza amua kutafuta vifaa tofauti tofauti vya kufanyia kazi kitaalamu zaidi.
19. Kocha wa mazoezi
Nathubutu kusema kuwa hakuna kitu chenye thamani kwenye maisha kama afya nzuri.
Watu wengi wanashtuka sikuhizi juu ya umuhimu wa kula vizuri na kufanya mazoezi. Hivyo, baada ya kupata elimu nzuri ya mazoezi, anza kawafundisha watu. Utalipwa kwa ujuzi na muda wako.
20. Kupamba maharusi
Harusi ni biashara kubwa.
Hivi, nani hapendi kupendeza siku ya harusi yake? Hamna. Na ili kupendeza harusini, wanandoa inabidi wapambwe.
Tafuta mtu anayepamba maharusi na muombe kumfanyia kazi (ikiwezekana bila hata malipo). Baada ya muda utajifunza vitu vingi vitakavyo kusaidia kuwa mtaalamu wa kupamba maharusi.
21. Kuwauzia watu bidhaa zao
Kwa akili ya kawaida, ni rahisi mtu kukulipa unapomtengenezea pesa.
Jifunze kuuza kisha tafuta watu wenye biashara na uwaambie kuwa unaweza kuwaletea wateja kwa malipo mutakayokubaliana.
Hii ni biashara nzuri kwasababu unatengeneza kipato kwa kutumia fedha ya mtu mwengine. Unachohitaji ni ujuzi wa kuuza vitu.
Hitimisho
Kama nilivyotangulia hapo awali kwa kusema; “hakuna biashara ndogo”.
Kinachofanya biashara ifanikiwe sio pesa, ni kujifunza, bidii, mbinu na kutokata tamaa katika safari yako hiyo. Jasho na muda ndio mtaji mkubwa na kila kizuri kina changamoto zake.
Hivyo, changamoto zitakapokuja kuwa na ujasiri wa kutafuta suluhisho lake. Ukiweza kufanya hivyo utapiga hatua.
Tuandikie maoni yako au kitu ulichokipenda kwenye kisanduku cha maoni hapa chini
4 Comments
MAONI YAKO NI MUHIMU TAFADHARI TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI